1Mwimbieni Mwenyezi Mungu wimbo mpya;mwimbieni Mwenyezi Mungu dunia yote.2Mwimbieni Mwenyezi Mungu, lisifuni jina lake;tangazeni wokovu wake siku baada ya siku.3Tangazeni utukufu wake katika mataifa,matendo yake ya ajabu miongoni mwa mataifa yote.4Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mkuu mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote;yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote.5Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu,lakini Mwenyezi Mungu aliziumba mbingu.6Fahari na enzi viko mbele yake;nguvu na utukufu vimo patakatifu pake.7Mpeni Mwenyezi Mungu, enyi jamaa za mataifa,mpeni Mwenyezi Mungu utukufu na nguvu.8Mpeni Mwenyezi Mungu utukufu unaostahili jina lake;leteni sadaka na mje katika nyua zake.9Mwabuduni Mwenyezi Mungu katika uzuri wa utakatifu wake;dunia yote na itetemeke mbele zake.10Semeni katika mataifa kwamba, “Mwenyezi Mungu anatawala.”Ulimwengu ameuweka imara, hauwezi kusogezwa;atawahukumu watu kwa uadilifu.11Mbingu na zishangilie, nchi na ifurahi;bahari na ivume, na vyote vilivyo ndani yake;12mashamba na yashangilie,pamoja na vyote vilivyomo.Kisha miti yote ya msituni itaimba kwa furaha;13itaimba mbele za Mwenyezi Mungu kwa maana anakuja,anakuja kuihukumu dunia.Ataihukumu dunia kwa haki,na mataifa katika kweli yake.