Mathayo27
Isa apelekwa kwa Pilato
1Asubuhi na mapema, viongozi wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri pamoja dhidi ya Isa ili kumuua.2Wakamfunga, wakampeleka na kumkabidhi kwa Pilato, aliyekuwa mtawala Mrumi.Yuda ajinyonga
3Yuda, aliyemsaliti Isa, alipoona kuwa Isa amehukumiwa, akajuta na akarudisha vile vipande thelathini vya fedha alivyopewa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu.4Akasema, “Nimetenda dhambi, kwa maana nimeisaliti damu isiyo na hatia.”Wakamjibu, “Hilo latuhusu nini sisi? Ni shauri yako.”5Basi Yuda akavitupa vile vipande vya fedha ndani ya Hekalu akaondoka akaenda kujinyonga.6Wale viongozi wa makuhani wakazichukua zile fedha wakasema, “Si halali kuchanganya fedha hizi na sadaka kwa sababu hizi ni fedha zenye damu.”7Hivyo basi, baada ya kushauriana, waliamua kuzitumia kununulia shamba la mfinyanzi, liwe mahali pa kuzikia wageni.8Hii ndiyo sababu lile shamba likaitwa Shamba la Damu hadi leo.9Ndipo likatimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, kwamba, “Walichukua vile vipande thelathini vya fedha, thamani aliyowekewa na watu wa Israeli,10wakanunulia shamba la mfinyanzi, kama vile Mwenyezi Mungu alivyoniagiza.”
Pilato amhoji Isa
11Wakati huo Isa akiwa amesimama mbele ya mtawala, mtawala akamuuliza, “Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi?”Isa akasema, “Wewe wasema hivyo.”12Lakini viongozi wa makuhani na wazee walipomshtaki, hakujibu neno.13Ndipo Pilato akamuuliza, “Je, husikii ni mambo mangapi wanayokushtaki nayo?”14Lakini Isa hakumjibu hata kwa shtaka moja, kiasi kwamba mtawala alishangaa sana.
Pilato amtoa Isa asulubiwe
15Basi ilikuwa ni desturi ya mtawala kumfungua mfungwa mmoja aliyechaguliwa na umati wa watu wakati wa sikukuu.16Palikuwa na mfungwa mmoja mwenye sifa mbaya, aliyeitwa Baraba.17Hivyo umati wa watu walipokusanyika, Pilato akawauliza hao watu, “Mnataka niwafungulie yupi: Baraba au Isa aitwaye Al-Masihi?”18Kwa kuwa alitambua kwamba walikuwa wamemkabidhi Isa kwake kwa ajili ya wivu.19Pilato akiwa ameketi kwenye kiti cha hukumu, mkewe akampelekea ujumbe huu: “Usiwe na jambo lolote juu ya mtu huyu asiye na hatia, kwa kuwa leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake.”20Lakini viongozi wa makuhani na wazee wakashawishi umati wa watu kwamba waombe Baraba afunguliwe, naye Isa auawe.21Mtawala akawauliza tena, “Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka niwafungulie?”Wakajibu, “Baraba.”22Pilato akawaambia, “Basi nifanye nini na huyu Isa aitwaye Al-Masihi?”
Wakajibu wote, “Msulubishe!”23Pilato akauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?”
Lakini wao wakazidi kupiga kelele, wakisema, “Msulubishe!”24Pilato alipoona kwamba hawezi kufanya lolote, lakini badala yake ghasia zilikuwa zinaanza, akachukua maji, akanawa mikono yake mbele ya umati wa watu, akasema, “Sina hatia kwa damu ya mtu huyu, hili ni jukumu lenu!”25Watu wote wakajibu, “Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu!”26Basi akawafungulia Baraba. Lakini baada ya kuamuru Isa apigwe mijeledi, akamtoa ili asulubishwe.
Askari wamdhihaki Isa
27Kisha askari wa mtawala wakampeleka Isa kwenye Praitorio , na wakakusanya kikosi kizima cha askari kumzunguka.28Wakamvua nguo zake na kumvika vazi la rangi nyekundu, kisha29wakasokota taji la miiba, wakaiweka kichwani pake. Wakamwekea fimbo katika mkono wake wa kuume, na wakapiga magoti mbele zake na kumdhihaki, wakisema, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!”30Wakamtemea mate, wakachukua ile fimbo wakampiga kichwani tena na tena.31Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakampeleka ili wakamsulubishe.Isa asulubishwa
32Walipokuwa wakienda, wakakutana na mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, nao wakamlazimisha kuubeba ule msalaba.33Wakafika mahali palipoitwa Golgotha (maana yake ni Mahali pa Fuvu la Kichwa).34Hapo wakampa Isa divai iliyochanganywa na nyongo ili anywe; lakini alipoionja, akakataa kuinywa.35Walipokwisha kumsulubisha, wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. [Hili lilifanyika ili litimie neno lililonenwa na nabii, “Waligawa nguo zangu miongoni mwao na vazi langu wakalipigia kura.”] 36Kisha wakaketi, wakamchunga.37Juu ya kichwa chake, kwenye msalaba, wakaandika shtaka lake hivi:Huyu ni Isa
Mfalme wa Wayahudi.38Wanyang’anyi wawili walisulubiwa pamoja naye, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wa kushoto.39Watu waliokuwa wakipita njiani wakamtukana huku wakitikisa vichwa vyao,40na kusema, “Wewe ambaye utalivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe mwenyewe basi! Kama wewe ni Mwana wa Mungu , shuka msalabani.”41Vivyo hivyo, viongozi wa makuhani, walimu wa Torati pamoja na wazee wakamdhihaki, wakisema,42“Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! Yeye ni mfalme wa Israeli! Ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini.43Anamwamini Mungu, basi Mungu na amwokoe sasa kama anamtaka, kwa maana alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu.’ ”44Hata wale wanyang’anyi waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana vivyo hivyo.