Marko8
Isa alisha wanaume 4,000
1Katika siku hizo, umati mkubwa wa watu walikusanyika tena. Kwa kuwa walikuwa hawana chakula, Isa akawaita wanafunzi wake akawaambia,2“Ninahurumia umati huu wa watu, kwa sababu sasa wamekuwa nami kwa muda wa siku tatu na hawana chakula.3Nikiwaaga waende nyumbani bila kula, watazimia njiani kwa sababu baadhi yao wametoka mbali.”4Wanafunzi wake wakamjibu, “Lakini hapa nyikani tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha?”5Isa akawauliza, “Mna mikate mingapi?”Wakajibu, “Tuna mikate saba.”6Akawaambia watu waketi chini. Akaichukua ile mikate saba na kushukuru, baadaye akaimega na kuwapa wanafunzi wake ili wawagawie watu. Wanafunzi wake wakafanya hivyo.7Walikuwa pia na visamaki vichache, Isa akavibariki, akawaamuru wanafunzi wake wawagawie watu.8Wale watu walikula na kutosheka. Baadaye wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu saba.9Watu waliokula walikuwa wapata elfu nne. Baada ya kuwaaga,10aliingia kwenye mashua pamoja na wanafunzi wake, akaenda sehemu za Dalmanutha.
Mafarisayo waomba ishara
11Mafarisayo wakaja, wakaanza kumhoji Isa. Ili kumtega, wakamwomba awaoneshe ishara kutoka mbinguni.12Akahuzunika moyoni, akawaambia, “Kwa nini kizazi hiki kinataka ishara? Amin nawaambieni, hakitapewa ishara yoyote.”13Kisha akawaacha, akarudi kwenye mashua, akavuka hadi ng’ambo.Chachu ya Mafarisayo na ya Herode
14Wanafunzi walikuwa wamesahau kuchukua mikate ya kutosha. Walikuwa na mkate mmoja tu kwenye mashua.15Isa akawaonya: “Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na ya Herode.”16Wakajadiliana wao kwa wao, na kusema, “Anasema hivi kwa sababu hatukuleta mikate.”17Isa, akifahamu majadiliano yao, akawauliza: “Mbona mnajadiliana kuhusu kutokuwa na mikate? Je, bado hamtambui wala hamwelewi? Je, mbona mioyo yenu ni migumu kiasi hicho?18Je, mna macho lakini mnashindwa kuona, na mna masikio lakini mnashindwa kusikia? Je, hamkumbuki?19Nilipoimega ile mikate mitano kwa watu elfu tano, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa mabaki?”Wakamjibu, “Kumi na viwili.”20“Je, nilipoimega ile mikate saba kwa watu elfu nne, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa mabaki?”
Wakamjibu, “Saba.”21Ndipo akawauliza, “Je, bado hamwelewi?”
Isa amponya Kipofu huko Bethsaida
22Wakafika Bethsaida na baadhi ya watu wakamleta mtu mmoja kipofu wakamsihi Isa amguse.23Isa akamshika mkono huyo kipofu akampeleka nje ya kijiji. Baada ya kuyatemea mate macho ya yule kipofu na kumwekea mikono, Isa akamuuliza, “Unaona chochote?”24Yule kipofu akaangalia, akasema, “Ninaona watu, wanaonekana kama miti inayotembea.”25Isa akamwekea tena mikono machoni. Kisha macho yake yakafunguka, kuona kwake kukarejea naye akaona kila kitu dhahiri.26Isa akamtuma nyumbani mwake, akamwambia, “Hata kijijini usiingie.”Petro amkiri Isa kuwa Al-Masihi
27Isa na wanafunzi wake wakaelekea vijiji vya Kaisaria-Filipi. Walipokuwa njiani, Isa akawauliza, “Watu husema mimi ni nani?”28Wakamjibu, “Baadhi husema wewe ni Yahya, wengine husema ni Ilya, na bado wengine husema wewe ni mmoja wa manabii.”29Akawauliza, “Je, ninyi mnasema mimi ni nani?”Petro akajibu, “Wewe ndiwe Al-Masihi .”30Isa akawaonya wasimwambie mtu yeyote habari zake.