Marko15
Pilato amhoji Isa
1Asubuhi na mapema, viongozi wa makuhani, pamoja na wazee, walimu wa Torati na Baraza la Wayahudi lote, wakafikia uamuzi. Wakamfunga Isa, wakamchukua na kumkabidhi kwa Pilato.2Pilato akamuuliza, “Je, wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi?”Isa akajibu, “Wewe umesema.”3Viongozi wa makuhani wakamshtaki kwa mambo mengi.4Pilato akamuuliza tena, “Je, huna la kujibu? Tazama ni mashtaka mangapi wanayaleta juu yako.”5Lakini Isa hakujibu lolote, hivyo Pilato akashangaa.
Pilato amtoa Isa asulubiwe
6Ilikuwa desturi wakati wa Sikukuu ya Pasaka kumfungulia mfungwa yeyote ambaye watu wangemtaka.7Wakati huo, mtu aliyeitwa Baraba alikuwa amefungwa gerezani pamoja na waasi wengine waliokuwa wametekeleza uuaji wakati wa maasi.8Umati ule wa watu wakamjia Pilato na kumwomba awafanyie kama ilivyokuwa desturi yake.9Pilato akawauliza, “Mnataka niwafungulie huyu mfalme wa Wayahudi?”10Kwa maana yeye alitambua kuwa viongozi wa makuhani walikuwa wamemtia Isa mkononi mwake kwa ajili ya wivu.11Lakini viongozi wa makuhani wakachochea umati ule wa watu wamwombe awafungulie Baraba badala yake.12Pilato akawauliza tena, “Basi mnataka nifanye nini na huyu mtu mnayemwita mfalme wa Wayahudi?”13Wakapiga kelele, wakisema, “Msulubishe!”14Pilato akawauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?”Lakini wao wakapiga kelele zaidi, wakisema, “Msulubishe!”15Pilato, akitaka kuridhisha umati ule wa watu, akawafungulia Baraba. Naye baada ya kuamuru Isa apigwe mijeledi, akamtoa ili asulubishwe.
Askari wamdhihaki Isa
16Askari wakampeleka Isa hadi kwenye ukumbi wa ndani wa jumba la kifalme, ndio Praitorio , wakakusanya kikosi kizima cha askari.17Wakamvalisha Isa joho la zambarau, wakasokota taji la miiba, wakamvika kichwani.18Wakaanza kumsalimu kwa dhihaka, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!”19Wakampiga kwa fimbo ya mwanzi tena na tena kichwani na kumtemea mate. Wakapiga magoti mbele yake, wakamsujudia kwa kumdhihaki.20Walipokwisha kumdhihaki, wakamvua lile joho la zambarau, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakamtoa nje ili wakamsulubishe.Isa asulubishwa
21Mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, baba yao Iskanda na Rufo, alikuwa anaingia mjini kutoka mashambani, nao wakamlazimisha kuubeba ule msalaba.22Kisha wakampeleka Isa hadi mahali palipoitwa Golgotha (maana yake ni Mahali pa Fuvu la Kichwa).23Nao wakampa divai iliyochanganywa na manemane, lakini hakuinywa.24Basi wakamsulubisha, nazo nguo zake wakagawana miongoni mwao kwa kuzipigia kura ili kuamua ni gani kila mtu ataichukua.25Ilikuwa saa tatu asubuhi walipomsulubisha.26Tangazo likaandikwa la mashtaka dhidi yake lenye maneno haya:Mfalme wa Wayahudi.27Pamoja naye walisulubiwa wanyang’anyi wawili, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wa kushoto. [28Nalo andiko likatimizwa, lisemalo, “Alihesabiwa pamoja na watenda dhambi.”] 29Watu waliokuwa wakipita njiani wakamtukana huku wakitikisa vichwa vyao na kusema, “Aha! Wewe ambaye utalivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu,30basi shuka kutoka msalabani na ujiokoe mwenyewe!”31Vivyo hivyo, viongozi wa makuhani pamoja na walimu wa Torati wakamdhihaki miongoni mwao wakisema, “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe!32Basi huyu Al-Masihi , huyu mfalme wa Israeli, ashuke sasa msalabani, ili tupate kuona na kuamini.” Wale waliosulubiwa pamoja naye pia wakamtukana.