Luka23
Pilato amhoji Isa
1Kisha umati wote wa watu wakainuka na kumpeleka Isa kwa Pilato.2Nao wakaanza kumshtaki wakisema: “Tumemwona huyu mtu akipotosha taifa letu, akiwazuia watu wasilipe kodi kwa Kaisari na kujiita ni Al-Masihi , mfalme.”3Basi Pilato akamuuliza Isa, “Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi?”Isa akajibu, “Wewe wasema.”4Pilato akawaambia viongozi wa makuhani na umati ule wote, “Sioni msingi wowote wa kumshtaki mtu huyu!”5Lakini wao wakakazana kusema, “Anawachochea watu kwa mafundisho yake katika Yudea yote, tangu Galilaya alikoanzia, hadi sehemu hii!”
Isa apelekwa kwa Herode
6Pilato aliposikia hayo akauliza kama huyo mtu alikuwa Mgalilaya.7Alipofahamu kwamba Isa alikuwa chini ya mamlaka ya Herode, akampeleka kwa Herode, ambaye wakati huo alikuwa pia Yerusalemu.8Herode alipomwona Isa alifurahi sana, kwa sababu kwa muda mrefu alikuwa amesikia mambo mengi kumhusu. Pia alitarajia kumwona akifanya miujiza kadha wa kadha.9Herode akamuuliza maswali mengi, lakini Isa hakumjibu lolote.10Wakati huo viongozi wa makuhani na walimu wa Torati walikuwa wakitoa mashtaka yao kwa nguvu sana.11Herode na askari wake wakamdhihaki Isa na kumfanyia mzaha. Wakamvika vazi zuri sana, wakamrudisha kwa Pilato.12Siku hiyo, Herode na Pilato wakapata urafiki; kabla ya jambo hili walikuwa na uadui kati yao.Isa ahukumiwa kifo
13Basi Pilato akawaita pamoja viongozi wa makuhani, viongozi wengine na watu,14akawaambia, “Ninyi mlimleta huyu mtu kwangu kana kwamba ni mtu anayewachochea watu ili waasi. Nimemhoji mbele yenu nami sikupata msingi wowote wa mashtaka yenu dhidi yake.15Wala Herode hakumpata na kosa lolote, ndiyo sababu amemrudisha kwetu. Kama mnavyoona, mtu huyu hakufanya jambo lolote linalostahili kifo.16Kwa hiyo nitaamuru apigwe mijeledi na kumwachilia.” [17Kwa kuwa ilikuwa lazima kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa Sikukuu.] 18Ndipo watu wote wakapiga kelele kwa pamoja, “Mwondoe mtu huyu! Tufungulie Baraba!”19(Baraba alikuwa amefungwa gerezani kwa sababu ya maasi yaliyokuwa yametokea mjini, na kwa ajili ya uuaji.)20Pilato, akitaka kumwachia Isa, akasema nao tena.21Lakini wao wakaendelea kupiga kelele wakisema, “Msulubishe! Msulubishe!”22Kwa mara ya tatu, Pilato akawauliza, “Kwani amefanya kosa gani huyu mtu? Sikuona kwake sababu yoyote inayostahili adhabu ya kifo. Kwa hiyo nitaamuru apigwe mijeledi, na kisha nitamwachia.”23Lakini watu wakazidi kupiga kelele kwa nguvu, wakidai kwamba Isa asulubiwe. Hivyo, kelele zao zikashinda.24Kwa hiyo Pilato akatoa hukumu kwamba madai yao yatimizwe.25Akamfungua yule mtu aliyekuwa amefungwa gerezani kwa kuhusika katika uasi dhidi ya serikali na mauaji. Akamkabidhi Isa mikononi mwao, wamfanyie watakavyo.Isa asulubishwa
26Walipokuwa wakienda naye, wakamkamata mtu mmoja aitwaye Simoni Mkirene, aliyekuwa anapita zake kuingia mjini kutoka shambani. Wakambebesha msalaba, wakamlazimisha auchukue nyuma ya Isa.27Idadi kubwa ya watu wakamfuata Isa, wakiwamo wanawake waliokuwa wakimlilia na kumwombolezea.28Isa akawageukia, akawaambia, “Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi bali jililieni ninyi wenyewe na watoto wenu.29Kwa maana wakati utafika mtakaposema, ‘Wamebarikiwa wanawake tasa, ambao tumbo zao hazikuzaa, wala matiti yao hayakunyonyesha!’30Ndipo“ ‘wataiambia milima, “Tuangukieni!”na vilima, “Tufunikeni!” ’31Kwa maana kama wamefanya hivi kwa mti mbichi, kwa mti mkavu itakuwaje?”32Watu wawili wahalifu walipelekwa pamoja na Isa ili wakasulubiwe.33Walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, hapo ndipo walimsulubisha Isa pamoja na hao wahalifu, mmoja upande wake wa kuume, na mwingine upande wake wa kushoto.34Isa akasema, “Baba , wasamehe, kwa maana hawajui walitendalo!” Wakagawana nguo zake kwa kupiga kura.35Watu wakasimama hapo wakimwangalia, nao viongozi wa Wayahudi wakamdhihaki wakisema, “Aliokoa wengine! Ajiokoe mwenyewe basi, kama yeye ndiye Al-Masihi wa Mungu, Mteule wake.”36Askari nao wakaja, wakamdhihaki. Wakamletea siki ili anywe,37na wakamwambia, “Kama wewe ni mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe.”38Kwenye msalaba juu ya kichwa chake, kulikuwa na maandishi haya:Huyu ndiye
Mfalme wa Wayahudi.39Mmoja wa wale wahalifu waliosulubiwa pamoja naye akamtukana, akasema: “Wewe si ndiye Al-Masihi? Jiokoe mwenyewe na utuokoe na sisi.”40Lakini yule mhalifu mwingine akamkemea mwenzake, akasema, “Je, wewe humwogopi Mungu, wakati uko kwenye adhabu hiyo hiyo?41Sisi tumehukumiwa kwa haki kwa kuwa tunapata tunayostahili kwa ajili ya matendo yetu. Lakini huyu mtu hajafanya kosa lolote.”42Kisha akasema, “Isa, unikumbuke utakapokuja katika ufalme wako.”43Isa akamjibu, “Amin, nakuambia, leo utakuwa pamoja nami Paradiso. ”