Luka16
Mfano wa msimamizi mjanja
1Isa akawaambia wanafunzi wake, “Palikuwa na tajiri mmoja na msimamizi wake. Huyo msimamizi alishitakiwa kwake kwamba alikuwa akitapanya mali ya tajiri yake.2Hivyo huyo tajiri akamwita na kumuuliza, ‘Ni mambo gani haya ninayoyasikia kukuhusu? Toa taarifa ya usimamizi wako, kwa sababu huwezi kuendelea kuwa msimamizi.’3“Yule msimamizi akawaza moyoni mwake, ‘Nitafanya nini sasa? Bwana wangu ananiondoa katika kazi yangu. Sina nguvu za kulima, nami ninaona aibu kuombaomba.4Najua nitakalofanya ili nikiachishwa kazi yangu hapa, watu wanikaribishe nyumbani mwao.’5“Kwa hiyo akawaita wadeni wote wa bwana wake, mmoja mmoja. Akamuuliza wa kwanza, ‘Deni lako kwa bwana wangu ni kiasi gani?’6“Akajibu, ‘Vipimo mia moja vya mafuta ya mizeituni.’“Msimamizi akamwambia, ‘Chukua hati ya deni lako, ibadilishe upesi, uandike vipimo hamsini.’7“Kisha akamuuliza wa pili, ‘Wewe deni lako ni kiasi gani?’
“Akajibu, ‘Vipimo elfu moja vya ngano.’
“Yule msimamizi akamwambia, ‘Chukua hati yako, uandike vipimo mia nane!’8“Yule bwana akamsifu yule msimamizi dhalimu kwa jinsi alivyotumia ujanja. Kwa maana watu wa dunia hii wana ujanja zaidi wanapojishughulisha na mambo ya dunia kuliko watu wa nuru.9Nawaambia, tumieni mali ya dunia kujipatia rafiki, ili itakapokwisha, mkaribishwe katika makao ya milele.10“Yeyote aliye mwaminifu katika mambo madogo, pia ni mwaminifu katika mambo makubwa. Na yeyote asiye mwaminifu katika mambo madogo pia si mwaminifu katika mambo makubwa.11Ikiwa hamkuwa waaminifu katika mali ya kidunia, ni nani atakayewaaminia mali ya kweli?12Nanyi kama hamkuwa waaminifu na mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe?13“Hakuna mtumishi awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali .”14Mafarisayo, waliokuwa wapenda fedha, waliyasikia hayo yote na wakamcheka kwa dharau.15Isa akawaambia, “Ninyi mnajionesha kuwa wenye haki mbele za wanadamu, lakini Mungu anaijua mioyo yenu. Kwa maana vile vitu ambavyo wanadamu wanavithamini sana, kwa Mungu ni machukizo.