Yoshua15swh_onmm
Mgawo kwa Yuda
1Mgawo kwa kabila la Yuda, ulienea kufuatana na koo zao, ukishuka kufikia eneo la Edomu, hadi Jangwa la Sini mwisho kabisa upande wa kusini.2Mpaka wao wa kusini ulianzia ghuba iliyo kwenye ncha ya kusini mwa Bahari ya Chumvi,3ukakatiza kusini mwa Akrabimu, ukaendelea hadi Sini, kisha ukaenda hadi kusini mwa Kadesh-Barnea. Tena ukapitia Hesroni, ukapanda hadi Adari, na ukapinda hadi Karka.4Kisha ukaendelea hadi Azmoni, na kuunganika na Kijito cha Misri, na kuishia baharini. Huu ndio mpaka wao wa upande wa kusini.5Mpaka wa upande wa mashariki ni Bahari ya Chumvi ukienea mahali Mto Yordani unapoingilia. Mpaka wa upande wa kaskazini ulianzia ghuba ya bahari mahali Mto Yordani unapoingilia,6ukapanda hadi Beth-Hogla, na kuendelea kaskazini mwa Beth-Araba hadi kwenye Jiwe la Bohani mwana wa Reubeni.7Kisha mpaka ulipanda hadi Debiri kutoka Bonde la Akori, na kugeuka kaskazini hadi Gilgali inayotazamana na miteremko ya Adumimu, kusini mwa bonde. Ukaendelea sambamba hadi maji ya En-Shemeshi na kutokeza huko En-Rogeli.8Kisha ukapanda kwa kufuata Bonde la Ben-Hinomu sambamba na mteremko wa kusini wa mji mkubwa wa Wayebusi (yaani Yerusalemu). Kutoka hapo ukapanda juu ya kilima magharibi mwa Bonde la Hinomu mwisho wa ncha ya kaskazini mwa Bonde la Warefai.9Kutoka juu ya kilima, mpaka ule ukaendelea hadi kwenye chemchemi ya maji ya Neftoa, ukatokea kwenye miji ya Mlima Efroni na kuteremka kuelekea Baala (yaani Kiriath-Yearimu).10Kisha ukapinda upande wa magharibi kutoka Baala hadi Mlima Seiri, ukafuatia sambamba mteremko wa kaskazini mwa Mlima Yearimu (yaani Kesaloni), ukashuka hadi Beth-Shemeshi, na kukatiza hadi Timna.11Ukaelekea hadi mteremko wa kaskazini mwa Ekroni, ukageuka kuelekea Shikeroni, ukapita hadi Mlima Baala na kufika Yabineeli. Mpaka ule ukaishia baharini.12Mpaka wa magharibi ni pwani ya Bahari Kuu.Hii ndiyo mipaka ya watu wa Yuda kwa koo zao.