Yeremia40
Yeremia aachiwa huru
1Neno likamjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi Mungu baada ya Nebuzaradani mkuu wa askari walinzi wa mfalme kumfungua huko Rama. Alikuwa amemkuta Yeremia akiwa amefungwa kwa minyororo miongoni mwa mateka wote kutoka Yerusalemu na Yuda waliokuwa wakipelekwa uhamishoni Babeli.2Mkuu wa askari walinzi alipomwona Yeremia, akamwambia, “Mwenyezi Mungu, Mungu wako, aliamuru maafa haya kutokea mahali hapa.3Sasa Mwenyezi Mungu ameyaleta haya, amefanya sawasawa na alivyosema angefanya. Yote haya yametokea kwa sababu ninyi mlifanya dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu na hamkumtii.4Lakini leo ninakufungua minyororo iliyo kwenye viwiko vya mikono yako. Ukiona ni vema, twende pamoja hadi Babeli; nami nitakutunza. Lakini kama hutaki, basi usije. Tazama, nchi yote iko mbele yako, nenda kokote unakotaka.”5Lakini kabla Yeremia hajageuka kuondoka, Nebuzaradani akaongeza kusema, “Rudi kwa Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani, ambaye mfalme wa Babeli amemchagua awe juu ya miji ya Yuda, ukaishi naye miongoni mwa watu, au uende popote panapokupendeza.”Kisha huyo kiongozi akampa posho yake na zawadi, akamwacha aende zake.6Kwa hiyo Yeremia akaenda kwa Gedalia mwana wa Ahikamu huko Mispa, na kuishi naye miongoni mwa watu walioachwa katika nchi.