Ezekieli37
Bonde la mifupa iliyokauka
1Mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa juu yangu, naye akanitoa nje kwa Roho wa Mwenyezi Mungu na kuniweka katikati ya bonde lililokuwa limejaa mifupa tele.2Akanipitisha pande zote kwenye hiyo mifupa, nami nikaona mifupa mingi sana ndani ya lile bonde, mifupa iliyokuwa imekauka sana.3Akaniuliza, “Mwanadamu, mifupa hii yaweza kuishi?”Nikajibu, “Ee Bwana Mungu Mwenyezi, wewe peke yako unajua.”4Ndipo akaniambia, “Itabirie mifupa hii na uiambie, ‘Enyi mifupa mikavu, sikieni neno la Mwenyezi Mungu!5Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi kwa hii mifupa: Nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi.6Nitawawekea mishipa, nami nitaifanya nyama ije juu yenu na kuwafunika kwa ngozi. Nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtakuwa hai. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”7Basi nikatabiri kama nilivyoamriwa. Nilipokuwa nikitabiri, kukawa na sauti, sauti ya kugongana, nayo mifupa ikasogeleana, mfupa kwa mfupa mwenziwe.8Nikatazama: mishipa na nyama vikatokea juu ya mifupa na ngozi ikaifunika, lakini haikuwa na pumzi ndani yake.9Ndipo aliponiambia, “Utabirie pumzi; tabiri, mwanadamu na uiambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Njoo kutoka pande nne za pepo, ee pumzi, nawe upulizie pumzi ndani ya hawa waliouawa, ili wapate kuishi.’ ”10Hivyo nikatabiri kama alivyoniamuru, nayo pumzi ikawaingia, wakawa hai na wakasimama kwa miguu yao, jeshi kubwa mno.11Ndipo akaniambia: “Mwanadamu, mifupa hii ni nyumba yote ya Israeli. Nao wanasema, ‘Mifupa yetu imekauka na tumaini letu limetoweka, tumekatiliwa mbali.’12Hivyo watabirie na uwaambie: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Enyi watu wangu, nitayafunua makaburi yenu na kuwatoa ndani yake, nami nitawarudisha tena katika nchi ya Israeli.13Ndipo ninyi watu wangu, mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nitakapoyafunua makaburi yenu na kuwatoa humo.14Nitatia Roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi; nami nitawakalisha katika nchi yenu wenyewe. Ndipo mtajua kuwa Mimi Mwenyezi Mungu nimenena, nami nitalitenda, asema Mwenyezi Mungu!’ ”